15.1 Utangulizi Katika muhadhara huu, tunakusudia kuelezea semantiki. Awali neno semantiki lilitumika kumaanisha sayansi ya “maana” kwa ujumla, hivi kwamba ilishughulikiwa na wanafilosofia, wanasaikolojia, wanamantiki, wanaanthropolojia na wengineo. Baadaye stadi hii ilijishughulisha zaidi na maana katika muktadha wa mwanadamu. Katika muhadhara huu tutashughulikia semantiki katika muktadha huu yaani maana katika misingi ya kinadharia ya isimu. Madhumuni ya Muhadhara Baada ya kumaliza kusoma muhadhara huu, mwanafunzi ataweza: (i) Kueleza maana ya maana (ii) Kuainisha aina za maana (iii) Kueleza na kutofautisha uhusiano wa maana (iv) Kueleza dhana ya maana kiutendaji 15.2 Maana Neno maana linafahiwa nyingi. Watu wa kawaida wamelitumia kumaanisha vitu mbalimbali: Una maana gani kwa kufika umechelewa Yale mawingu meusi yana maana mvua itanyesha sasa hivi Hiyo nguo nyekundu inamaanisha hatari Mradi huu una maana kubwa “Baba” maana ...