MAANA YA SEMANTIKI, MAANA YA MAANA
- Get link
- X
- Other Apps
15.1 Utangulizi
Katika muhadhara huu, tunakusudia kuelezea semantiki. Awali neno semantiki lilitumika kumaanisha sayansi ya “maana” kwa ujumla, hivi kwamba ilishughulikiwa na wanafilosofia, wanasaikolojia, wanamantiki, wanaanthropolojia na wengineo. Baadaye stadi hii ilijishughulisha zaidi na maana katika muktadha wa mwanadamu. Katika muhadhara huu tutashughulikia semantiki katika muktadha huu yaani maana katika misingi ya kinadharia ya isimu.
Madhumuni ya Muhadhara
Baada ya kumaliza kusoma muhadhara huu, mwanafunzi ataweza:
(i) Kueleza maana ya maana
(ii) Kuainisha aina za maana
(iii) Kueleza na kutofautisha uhusiano wa maana
(iv) Kueleza dhana ya maana kiutendaji
15.2 Maana
Neno maana linafahiwa nyingi. Watu wa kawaida wamelitumia kumaanisha vitu mbalimbali:
- Una maana gani kwa kufika umechelewa
- Yale mawingu meusi yana maana mvua itanyesha sasa hivi
- Hiyo nguo nyekundu inamaanisha hatari
- Mradi huu una maana kubwa
- “Baba” maana yake MZAZI WA KIUME
Maana inayoyorejelewa katika lugha ni ile katika sentensi ya “e”. Dhana ya maana ni ya kidhahania kwa sababu haina muundo thabiti kama vile viambajengo vya lugha kama vile vya: kifonolojia, kimofolojia au kisintaksia. Maana pia hutegemea dhamira ya mtoa ujumbe na fasiri ya mpokea ujumbe.
15.3 Aina za Maana
Wanaisimu mbalimbali wameeleza dhana ya aina za maana katika vitengo viwili vikuu; maana ya msingi na maana ya ziada. Hata hivyo Leech (1981) amebainisha aina za maana zifuatazo:
15.3 1 Maana ya msingi (conceptual meaning)
– Hii ni aina ya maana ambayo haibadiliki mfano; mwanamke, mwanaume. Hutaja sifa zake kuu. Zile sifa bainifu ndizo hupelekea kupata maana kuhusu mtu.
15.3.2 Maana dokezi (connotative meaning)
– Ni aina ya maana ambayo hutokana na umbo la kitu, kisaikolojia, kimatamshi mf. Kiumbo kushika mimba, kisaikolojia umama.
15.3.3 Maana ya kijamii / kimtindo (social meaning)
– Ni aina ya maana ambayo hupatikana kutokana na mazingira ya kijamii, wakati, utamaduni, kijiografia, kiuwasilishaji, hadhi, ubinafsi n.k
15.3.4 Maana ya kihisi (emotive meaning)
– Ni maana za kihisia ambazo hutokana na upotoshaji wa aina fulani wa maana ya msingi. Ni maana itokanayo na utumizi usio wa moja kwa moja ili kutoa maana. Maana ya kitu huwa ni ya mzunguko, fiche, kwa mfano maana za hisia hutegemea sana Kiimbo kiwekwacho katika neno au Kiimbo kiwekwacho katika sentensi.
15.3.5 Maana ambatani (collocative meaning)
– Maana ambatani au tangamano, ni aina ya maana itokanayo na utangamano au uambatani wa baadhi ya maneno kwa mfano: Mrembo – Msichana
: Ujamali – Mvulana
: Jitu hili ni la miraba mine – Mwanaume
– Katika lugha maneno pia hujengwa kwa mtindo huo mifano zaidi Samaki – Kiumbe wa majini/baharini au Swala – Kiumbe wa msituni. Ukitaja kimoja tu mfano samaki unakuwa umekiondoa kingine swala.
15.3.6 Maana ya kidhima/kidhamira (thematic meaning)
– Hizi ni aiana za maana ambazo ujumbe wake unapangwa kufuatana na msisitizo wa kitu. Maana hutokana na dhamira ambayo msemaji alikusudia ili imfikie msikilizaji, kwa mfano sentensi zifuatazo:
– (a) Mwalimu amempiga mtoto (Mwl. Mtenda)
– (b) Mtoto amepigwa na mwalimu (Mtoto Mtendwa)
– (c) Msichana yupo darasani (Jibu la swali lililoulizwa) – Msichana yuko wapi?
– (d) Darasani kuna msichana (Swali)
15.3.7 Maana akisi/Kimwangwi (reflected meaning)
– Ni maana ambazo ukitaji kitu fulani au maana fulani unakonyeza maana nyingine. Maana akisi haziachani kwa mfano: Jamii – Mkusanyiko wa watu pamoja
15.4 Uhusiano wa Maana
Katika taaluma ya semantiki, kuna uhusiano wa aina tatu wa maana; Utajo, Urejeleo na Fahiwati.
15.4.1 Utajo (Notion).
Huu ni uhusiano wa maana kutokana na kutaja kitu kama kilivyo katika ulimwengu halisi. Utajo hutaja kitu kama kilivyo kwa ujumla. Kwa mfano dhana ya meza katika ulimwengu huu tunaoufahamu maana zake ni nyingi lakini kuna sifa za kisemantiki zinazotofautisha meza na kitu kingine katika utamaduni. Kamusi moja (D. Crystal (1991: 97)* ilifafanua kuwa maana ya utajo ni sawa sawa na maana ya Kiurejeleo. Katika kubainisha maana kiutajo, rejelea sifa za kisemantiki unazozifahamu kimalimwengu. Mfano Mwanaume au Mwanamke (taja sifa za kila mmoja).
Utajo huhusu uhusiano baina ya leksimu au kipashio cha kiisimu na seti ya vitu ambayo inarejelewa na kipashio hicho katika ulimwengu halisi. Kwa mfano, utajo wa leksimu meza ni vitu vyote katika dunia ambavyo kwa hakika vinaitwa meza. (Kama nilivyosema, wataalamu wengine wanauita uhusiano huu urejeleo pia, lakini huku ni kuchanganya dhana!).
15.4.2 Fahiwati (Sense)
Fahiwa ya kiyambo ni seti ya mahusiano yaliyopo baina ya kiyambo hicho na viyambo vingine katika lugha. Mahusiano hayo huitwa mahusiano ya kifahiwa au ya kisemantiki. Mifano ya mahusiano hayo ni usawe (k.m. mwanaume, rijali), unyume (utu, unyama), n.k. Mahusiano hayo ndiyo yanayoukilia fahiwa ya kiyambo chochote kile.
Swali:
Je,“fahiwa” ina uhusiano gani na “utajo”? Dhana hizi zinatofautianaje na zinafananaje?
Tofauti baina ya fahiwa na utajo ni kwamba fahiwa ni uhusiano baina ya viyambo vya kileksia – yaani uhusiano ulio ndani ya lugha – wakati utajo ni uhusiano baina ya viyambo vya kileksia na seti ya vitu vilivyo duniani.
Ufanano baina ya fahiwa na utajo unaweza kuelezwa ifuatavyo. Dhana hizi kwa pamoja hutumika kwa viyambo sahili vya kileksia na viyambo changamani vya kileksia ambavyo fahiwa na utajo wake hutegemea fahiwa na utajo wa leksimu zinazounda viyambo hivyo. Kwa mfano, “mwanamke” ni kiyambo sahili wakati “mwanamke aliyezaa mtoto” ni kiyambo changamani. Fahiwa na utajo wa viyambo hivi unategemea fahiwa na utajo wa leksimu zinazoviunda.
Uhusiano mwingine uliopo baina ya fahiwa na utajo ni ule wa kutegemeana – yaani haiwezekani kufahamu fahiwa pasipo kufahamu utajo.
Uhusiano mwingine uliopo kati ya fahiwa na utajo ni ule ambao twaweza kuuita uhusiano pindu, ambao waweza kuelezwa ifuatavyo: iwapo utajo unazingatia dhana pana (yaani “utajo ni mkubwa”), basi fahiwa huwa ni finyu (yaani “dhana ndogo”). Tutatumia mfano wa mnyama na paka kuelezea jambo hili. Utajo wa “mnyama” ni mkubwa (yaani unzangatia viumbe wengi zaidi); fahiwa ya “mnyama” inajumuiza “paka” (paka wote ni wanyama, ila wanyama wote si paka) lakini si mahususi, na inaingizwa katika fahiwa ya “paka”.
* D. Crystal 1991. A DICTIONARY OF LINGUISTICS AND PHONETICS, TOLEO LA 3. Oxford: Blackwell.43
15.4.3 Urejeleo (Reference)
Urejeleo ni uhusiano baina ya viyambo vya kiisimu na viwakilisho vyake duniani wakati maalumu wa semo. Ni kipengele cha maana ya semo kinachotegemea muktadha. Masafa ya urejeleo ya viyambo rejelezi hutegemea utajo na fahiwa, lakini urejeleo halisi wa viyambo hivyo hutegemea mambo kadhaa yahusianayo na muktadha. Mfano wa viyambo rejelezi ni Machumu, mtoto yule, kijana aliyekuja sasa hivi, n.k. Sifa bainifu ya viyambo hivi vyote ni kwamba vinarejelea kitu mahususi katika ulimwengu wa masilugha, na kwamba vitu hivi vinaukiliwa na muktadha.
15.5 Viwango vya Maana
Dhana ya maana ni dhana ya kidhahania, hivyo wataalamu wa isimu wamejaribu kueleza dhana hii kiutendaji. Kiutendaji maana inaweza kubainishwa katika kiwango cha neno na kiwango cha tungo/sentensi.
(a) Maana katika Kiwango cha neno (Maana ya Kileksika)
– Hizi nia aina za maana zinazowakilishwa na vidahizo katika kamusi. Vidahizo hivi ni kwa mfano maeno kama vile “gari”, “mtu”, “barabara”. Maana kileksika pia hujulikana kama maana ya msingi. Maana msingi ndiyo maana kuu ya neno. Maana hii kwa kawaida huwa haibadiliki kutegemea athari za kimazingira au muktadha.
– Aina nyingine ya maana ya kileksikaa, ni ile maana kisarufi. Hii hurejelea maana ya neno katika muktadha wa matumizi
(b) Maana katika Kiwango cha Tungo
Tungo ni matokeo ya kuweka au kupanga pamoja vipashio sahili ili kujenga vipashio vikubwa zaidi vyenye maana. Mpangilio huo huzingatia kanuni fulani za kisarufi ili kuleta maana. Ukibadilisha uunganifu huo, maana nayo kadhalika hubadilika. Maana hupatikana kutokana na mpangilio kubalifu wa vipashio. Maana za tungo au sentensi hutawaliwa na kanuni ya utungamanifu.
Kanuni ya Utungamanifu: Miongoni mwa mambo yanayoukilia maana ya sentensi ni kanuni ya utungamanifu: kanuni inasema kwamba maana ya kiyambo changamani cha kisintaksia (kirai, sentensi) inatokana na maana za viambajengo vya kiyambo hicho na mpangilio au mahusiano yao ya kisarufi.
Umuhimu wa kanuni hiyo unadhihirika pindi maneno yaleyale yanapotumika kuunda sentensi zenye maana tofauti kutokana na tofauti za kimpangilio zilizojikita kwenye tofauti za mahusiano ya kisarufi. Chunguza mifano ifuatayo:
- Msichana alimkimbia mbwa
- Mbwa alimkimbia msichana
Tofauti baina ya sentensi (1) na (2) inatokana na nomino mbwa na msichana kubadilishana nafasi za kiima na yambwa. Hapa tunaona kuwa tofauti za mahusiano ya kisarufi zinazotokana na tofauti za mpangilio wa maneno huchangia katika maana ya sentensi.
Sifa na Mahusiano ya Kimaana
Baadhi ya sifa na mahusiano muhimu ya kimaana kwenye kiwango cha sentensi ni:
- Usawe
- Utata
- Ukinzani
- Upotoo
- Uziada-dufu
Usawe
Huu ni uhusiano baina ya sentensi mbili ua zaidi zenye kudhihirisha maana moja ya msingi. Mifano ya usawe ni hii ifuatayo:
- Kasoga alitupa jiwe likampiga Kwezi.
- Kasoga alivugumiza jiwe likamnasa Kwezi.
Katika mifano hii, vitenzi tupa na vugumiza vina maana ileile, na vitenzi piga na nasa vina maana ileile.
Usawe wa sentensi unafanana na usawe wa maneno kwa kuwa ni mahusiano yanayodhihirisha “uchopezi” bila badiliko la maana ya msingi.
Upo usawe wa namna mbili:
- Usawe wa kileksia
- Usawe wa kimuundo
Usawe wa kileksia unahusu sentensi mbili au zaidi ambazo zina maneno yenye maana ileile ya msingi katika nafasi ileile. Mifano (3) na (4) ni ya usawe wa namna hii.
Usawe wa kimuundo unatokana na maana ya msingi ya sentensi mbili au zaidi kubaki ileile japo sentensi zina mpangilio tofauti. Usawe huu ni wa kimuundo kwa sababu hauhusiani na usawa wa maana za maneno au virai – kwani maneno ama ni yale yale au yanatofautiana kidogo sana. Mifano:
- (a)Hakuna aliyeelewa maneno yake ya ajabu.
(b) Maneno yake ya ajabu hayakueleweka.
- (a) Maelezo yake yalikuwa magumu kufahamika.
(b) Ilikuwa vigumu kufahamu maelezo yake.
Sentensi (a) na (b) katika (5) na (6) zina maana ileile ya msingi. Sentensi za namna hii hutokana na mchakato ambao kiisimu huitwa uhamishaji. Mchakato huu huhamisha vipashio kadha toka mwishoni na kuvipeleka mwanzoni, na vya mwanzoni kuvipeleka mwishoni.
Utata
Utata ni kipengele kinachodhihirisha tafsiri zaidi ya moja. Upo utata wa kileksia na wa kimuundo.
Utata wa kileksia unatokana na polisemia au homonimia, kwa mfano:
- Baada ya shida nyingi alifanikiwa kumleta papa nyumbani.
- Bei ya kanga ni shilingi elfu nne.
Katika sentensi ya (7) papa anaweza kuwa papa mnyama au papa mkuu wa kanisa katoliki, na katika sentensi ya (8) kanga anaweza kuwa kanga ndege au kanga nguo.
Utata wa kimuundo unatokana na jinsi sentensi ilivyopangiliwa au umbo, neno au kirai kuwa katika nafasi maalumu ya sentensi. Mifano ni:
- Wanawake na wanaume waangalifu walikaa kando.
- Alimwandikia barua baba yake.
- Walipigana nasi.
Katika sentensi ya (9) tafsiri ni mbili: ama wanawake waangalifu na wanaume waangalifu au anawake na wanaume waangalifu. Katika sentensi ya (10) tafsiri ni mbili pia: ama aliandika barua kwa ajili au kwa niaba ya baba yake; au aliandika barua kwa baba yake. Na sentensi ya (11) ni tata: tafsiri ni ama: walipigana katika kundi letu dhidi ya adui yetu au walipigana dhidi yetu.
Usawa na utata vina uhusiano linganuzi. Katika usawe tungo kadhaa hupewa tafsiri moja, wakati katika utata tungo moja hupewa tafsiri zaidi ya moja. Uhusiano huu unaweza kuwakilishwa kama ifuatavyo:
Maana 1
Maana 2
UTATA WA TUNGO TUNGO 1 Maana 3
Maana 4
Maana …
Tungo 1
Tungo 2
USAWE WA TUNGO Tungo 3 MAANA 1
Tungo 4
Tungo…
Ukinzani
Kiyambo kinzani ni kile kinachodhihirisha vigambe viwili siganifu wakati mmoja. Kiyambo cha namna hii hunena kwamba fulani au kitu fulani kina sifa fulani na wakati huohuo hakina sifa hizo. Mifano ya viyambo kinzani ni:
- Yule mwanamme ni mwanamke.
- Yule mtu mzima ni mtoto.
- Hapo juu ndio chini.
Vigambe vinavyotolewa na sentensi hizo havikubaliani na ujuzi wetu wa malimwengu. Kwa mfano, mtu hawezi kuwa [+ME] na [-ME] wakati huohuo. Mifano mingine ya ukinzani ni:
- Nilishuka juu, nikapanda chini.
- Nilikwenda mbele, nikabaki nyuma.
Ukinzani kama huu hutumiwa sana na baadhi ya washairi wanapotaka kueleza jambo ambalo lina ukinzani ndani yake.
Upotoo
Huu ni ukiushi wa kisemantiki utokeao pindi vijenzi-semantiki viwili siganifu vinapounganishwa kueleza jambo au kitu.
Mifano ya upotoo ni:
- Alichora barua kwa mguu wa kushoto.
- Alimpiga teke kwa kalamu nyeusi.
Hapa upotoo unadhihirika baina ya chora na barua, na baina ya chora na mguu; kadhalika upo baina ya piga teke na kalamu.
Uziada-dufu
Uziada-dufu ni urudiaji usiohitajika; tazama mifano ifuatayo:
- Mke wangu ni mke wangu.
- Mbwa ni mnyama.
- Wanafunzi ni wanafunzi.
- Walimu ni walimu.
Kuna mambo mawili ambayo ni muhimu kuyataja kuhusiana na uziada-dufu:
- Ni urudiaji usio na jambo jipya; wala hauufanyi ujumbe ukawa wazi.
Sentensi yenye uziada-dufu ni kweli kwa mujibu wa maana za maneno yanayoiunda.
- Get link
- X
- Other Apps
Comments
Post a Comment
Tafadhari usicomment matusi