TANZU ZA USHAIRI WA KISWAHILI
Ushairi wa Kiswahili waweza kuainishwa katika tanzu au kumbo mbalimbali. Mulokozi (1996), ameuainisha ushairi wa kimapokeao katika kumbo kuu tatu za kimtindo. Kumbo hizo ni: ushairi wa kijadi au kimapokeo; ushairi wa mlegezo; na ushairi wa maigizo. 1. Ushairi wa Kimapokeo Haya ni mashairi ya kijadi yenye kufuata kanuni za urari wa mizani na mpangilio wa vina vya mwisho na/au vya kati. Mfano wa shairi la kimapokeo ni huu hapa: Namshukuru Namshukuru Illahi, Mwenyezi mkamilifu, Kwa kuishi nikawahi, kazini kustaafu, Bado ningali sahihi, imara na mkunjufu, Alihamdulilahi, namshukuru Latifu. Ulimwengu wa rakadha, umejaa hitilafu, Sikuweza mambo kadha: karibu mambo elfu; Kanipa hii karadha, Bwana Mungu namsifu, Alihamdulilahi, namshukuru Latifu. Hii sikutazamia, kwamba litanisadifu, Bahati imenijia, kwa kupenda Mtukufu, Mfano kama ruia, Mungu hana upungufu, Alihamdulilahi, namshukuru Latifu. (Shaaban Robert, 2003: 102 – 104) 2. Ushairi wa Mlegezo Haya ni mashairi...